
Sitaki kujifananisha na mtu wa aina yoyote ama kuungana na mtu yoyote katika mawazo yake juu ya maswahibu haya yaliyompata kijana mwenzetu *KANUMBA
Sitaki kumlaumu bwana Kanumba kama ‘wafanyavyo wengine wengi, nisingependa pia kuwalaumu wale wanaomlaumu kwa kuwa labda wameona kuna kosa katika kile alichokifanya (kubonga ung’eng’e ki-nursery). Uups. Kwa namna Fulani wote (*Kanumba na wanaomcheka) naona wanakosea tu.
KIVIPI BASI;
Alhamisi iliyopita ya tarehe 10/09/2009 niliyanukuu maneno ya Mrisho Mpoto aliyoyaimba katika nyimbo yake ya NIKIPATA NAULI yanayosema; "KUFUMBATIA MAJI KAMA JIWE, NI UJINGA". Nikayafananisha maji na lugha ngeni ikiwemo Kiingereza na nikasema ili tusifananishwe na Wajinga ni lazima tuishikilie lugha yetu (Kiswahili) ambayo niliifananisha na jiwe. Kwa kusema ukweli toka moyoni mwangu sikuwa na habari juu ya nini kinachoendelea huko BIG BROTHER.
Nimesikitika sana kusikia Ndugu yangu, Kipenzi changu *Kanumba amefanishwa na Mjinga kutokana na ‘kufumbatia maji kama jiwe’ hatimaye maji yamekauka na ameambulia sifa hasi (-) ambazo zimesababisha malumbano ya hapa na pale baina ya Wasanii wa Filamu na Wasanii wengine ama Wasanii wa filamu na Wanahabari.
Mimi ni mpenzi na mdau wa sanaa za maigizo na ninasema hivi TUSIPOJIANGALIA HATUTOFIKA TUTAKAPO.
Ninaamini kabisa kama *Kanumba asingejaribu kuyatumia yale MAJI watumiaji wa JIWE wasingethubutu kumlaumu na hata kulumbana.
Kosa la *KANUMBA ni kuisahau lugha yake alipoenda huko mbele za watu na kutaka kuzungumza Kiingereza ambacho kwa namna moja ama nyingine angekizungumza hapa kwetu hakuna ambaye angemlaumu na kuona kuwa amekosea.
Pichani *Kanumba akiwa HOLLYWOOD
Nini walichokosea wanaomlaumu?
Hatukupaswa kumlaumu *Kanumba kwa kukosea kuongea lugha ile ya wenyewe (Kiingereza) bali tulipaswa kumfariji na kumuomba ama kumtia nguvu na kumtaka awekee mkazo lugha yetu (Kiswahili) mara kwa mara aendapo mbele ya watumia lugha nyingine isiyokuwa ya Kiswahili. Ilitupasa kumshawishi *Kanumba kutumia Kiingereza katika FILAM kwani kule kila kitu kinaonekana kimepangwa hakuna ambaye atang’amua udhaifu wake katika lugha.
Hebu turudi nyuma kidogo ili tuwe na mfano hai katika hili, Katika Filamu moja ambayo iliwakutanisha wasanii toka Nigeria na Tanzania (DAR TO LAGOS) kuna sehemu moja *Kanumba alikaribishwa chakula naye baada ya kula akang’aka kuwa chakula kile hakiliki kwa kuwa kilikuwa na pilipili nyingi (THIS FOOD IS TOO MUCH PILIPILI), hii ilikuja kuwa ni kibwagizo katika vibwagizo vya filamu hiyo na kujizolea sifa zaidi. Mimi sijui kama ilipangwa sehemu hiyo itamkwe hivyo ama ndio…..
Naomba niwashukuru wadau na kuwahasa kuwa ni vyema kukumbatia lugha yetu pindi tukutanapo na wageni, kwani hii itasaidia kukuza lugha yetu na kuifanya iwe juu.
Nawatakia IDDIE NJEMA.

No comments:
Post a Comment